Akizungumza katika mdahalo huo, Sheikh Dkt. Al-Hadi Mussa Salum, Mwenyekiti wa JMAT, alisema: "Uchaguzi ni fursa ya kuonyesha uzalendo na kuchagua viongozi kwa njia ya amani".
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Leo hii, Tarehe 20 Agosti, 2025, umefanyika Mdahalo Mkubwa na Muhimu wa Kitaifa ulioratibiwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kushirikiana na Global Peace Foundation. Lengo la Mdahalo huo lilikuwa ni kujadili Amani, Haki na Siasa Safi kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Mdahalo huo ulihudhuriwa na viongozi wa dini, vyama vya siasa, vyombo vya habari, mashirika ya kiraia, taasisi za serikali na zisizo za serikali, wanawake na watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika mdahalo huo, Sheikh Dkt. Al-Hadi Mussa Salum, Mwenyekiti wa JMAT, alisema kuwa:
Uchaguzi ni fursa ya kuonyesha uzalendo na kuchagua viongozi kwa njia ya amani.
Lengo kuu ni kuelimisha wananchi, kupunguza mvutano wa kisiasa na kusisitiza ukweli, uwazi na kufuata sheria.
JMAT inalenga kudumisha amani na maridhiano bila kujali dini, mila, rangi au itikadi za kisiasa.
Mdahalo huu ni kielelezo cha ukuaji wa demokrasia nchini, kwani umekutanisha dini na siasa kwa pamoja kujadili mustakabali wa taifa.
Sheikh Dkt. Al-Hadi alisisitiza umuhimu wa:
1_Heshima kati ya wagombea na wapiga kura ili kuepusha siasa za chuki.
2_Tume ya Uchaguzi, vyombo vya usalama na mahakama kufanya kazi kwa uadilifu.
3_Vyombo vya habari kuripoti kwa uaminifu, kuchunguza taarifa kabla ya kuzitoa na kutoa jukwaa la wazi la majadiliano ya sera.
Mdahalo huu umetajwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa katiba ya JMAT, yenye malengo ya kuimarisha mshikamano wa kitaifa na maendeleo ya kijamii na kitaifa kwa misingi ya amani na utulivu.
Your Comment